Advertisement

Breaking

Wednesday, August 31, 2016

Macho yote duniani yapo Mbarali leo


Mnajimu wa Mambo ya Anga, Dk Noorali Jiwaji (kushoto) akiwaonyesha waandishi wa habari kifaa maalumu cha kuzuia mionzi ya jua ikiwa ni matayarisho ya kushuhudia tukio la kupatwa kwa jua wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya. Kulia Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete. 

Mbarali. Hali ya maisha imeanza kubadilika kwa wakazi wa mji wa Rujewa wilayani hapa Mkoa wa Mbeya kutokana na wingi wa wageni waliofika kushuhudia tukio la kihistoria la kupatwa kwa jua. Mara ya mwisho kutokea nchini ilikuwa mwaka 1977.

Baadhi ya maeneo yatashuhudia giza huku mengine yakishuhudia kufifia kwa mwanga wa jua. Kupatwa kwa jua kunatokea kama dunia, mwezi na jua kukaa kwenye mstari mmoja mnyoofu yaani wakati mwezi unapita kati ya dunia na jua.

Jua linapatwa leo, na wataalamu wa masuala ya anga wamelichagua eneo la Rujewa kwa ajili ya kuratibu mabadiliko hayo yanayotarajiwa kuanza kuonekana kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana.

Baadhi ya wageni kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi waliofika Rujewa na maeneo ya jirani kama Igawa, wanahaha kupata vyumba kwani vingi vimejaa huku wengine wakipandisha bei ya vyumba baada ya kugundua kuwa kutakuwa na wateja wengi.

Katika nyumba ya wageni ya Lugelele iliyopo mji mdogo wa Rujewa, mhudumu Juliana Mkung’a alisema vyumba vyote vimejaa na kulazimika kuwarudisha wageni ambao hajawahi kushuhudia tangu aanze kazi miaka sita iliyopita katika eneo hilo.

“Wageni tumewarudisha wengi kwa maana hatuna pa kuwaweka kuanzia jana (juzi) na leo (jana). Wageni wamekuja kwa ajili ya hili tukio la kupatwa kwa jua kesho (leo), ” alisema Juliana, mama wa mtoto mmoja.

Alisema biashara imechanganya msimu huu, hususan katika kipindi ambacho maisha yamekuwa magumu na fedha imekuwa ngumu, kitu ambacho kimewafanya kuona kupatwa kwa jua kuwa ni fursa kwao ya kutengeneza fedha.

Christopher Nyenyembe, mkazi wa Mbeya Mjini aliyefika Rujewa kwa ajili ya tukio la kupatwa kwa jua alihaha kupata sehemu ya kulala, huku akieleza kuwa sehemu nyingine bei zimepanda kwa kuwa wenyeji wanataka kutumia fursa hiyo kujipatia kipato cha ziada.

“Nilienda gesti ya Samunge, kumejaa, nikaenda Lugelele nako kumejaa. Tukio hili limesababisha ujio wa watu wengi,” alisema Nyenyembe.

Alisema wengine wameamua kupandisha bei za vyumba kutoka Sh15,000 na 20,000 na kuwa kati ya Sh25,000 na Sh30,000.

Wafanyabiashara wa chakula maarufu kama mamalishe, baadhi wameanza kuona mabadiliko katika biashara zao kwa ongezeko la wateja.

Hanifa Halifa, mamalishe katika kituo cha mabasi cha Rujewa alisema mabadiliko kiasi katika biashara yake yameanza kuonekana, lakini leo ana matarajio makubwa kwani wengi watakuja kushuhudia tukio la kihistoria.

Madereva wa bodaboda katika kituo cha mabasi Rujewa walieleza kuwa wataitumia fursa hiyo na tayari wameanza kupata wateja wanaouliza ama kwenda eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kutazama kupatwa kwa jua.

Mwakilishi wa waendesha bodaboda katika eneo hilo, Shabaan Kanevanu alisema leo wamejipanga na wameimarisha vyombo vyao ili kuhakikisha wanakabiliana na idadi ya wageni watakaofika Rujewa.

Ofisa Tarafa ya Rujewa, Sosteness Valerian alisema usalama umeandaliwa katika eneo la tukio na Serikali imejipanga kwa huduma za kibinadamu, kama huduma ya kwanza.

“Kuna mwingiliano mkubwa wa watu …gesti zimejaa lakini ulinzi umeimarishwa vya kutosha na watu wanataarifiwa wawe makini siku ya tukio kwani watapata athari kwenye macho,” alisema ofisa huyo.

Alisema utaratibu kwa wanafunzi umeandaliwa na vifaa vya kukinga macho 100 vitatumiwa kwa kupokezana ili waweze kujifunza kwa vitendo.

Wanafunzi wa Shule ya Ibara waliielezea Mwananchi kuwa tukio hilo litawasaidia kujifunza.

“Hata kwenye mtihani baada ya kuona tukio hilo, sitaweza kukosea swali litakalotokana na kupatwa kwa jua. Kwangu ni historia kubwa kushuhudia tukio hilo,” alisema Evidence Mahenge, mwanafunzi wa darasa la saba Ibara.

Mwalimu wa Jiografia Shule ya Msingi Ibara, Nuru Said alisema tukio hilo litawasaidia kufundisha mada ya kupatwa kwa jua kwa vitendo tofauti na sasa msaada mkubwa wanaotumia ni michoro.

Gari la matangazo”Tangazo, tangazo, tangazo kesho (leo) jua litapatwa hivyo wananchi mnakaribishwa kwenda kuangalia tukio la jua kupatwa Rujewa karibu na ofisi za Halmashauri ya Mbarali …mnatakiwa msiangalie juu kwani mpatapa madhara,” ni sauti ya gari la matangazo likikatisha katika viunga vya mji wa Rujewa.

Hata hivyo, licha ya baadhi kuona tukio hilo ni la kihistoria, baadhi wanahofu kuwa huenda litakuwa na madhara kwao.

Wende Kiswaga, muuza matunda kituo cha mabasi cha Rujewa alisema baadhi yao wameanza kuhofia huenda ni tukio lenye madhara kwao.

“Wengi wetu tunajua labda dunia itakwisha. Lakini kinachotupa moyo ni kuwa wageni wanakuja wengi hivyo sidhani kuwa wangependa kudhurika,” alisema mjasiriamali huyo.

Changamoto

Pamoja na kuwa huduma za kulala wageni hazitoshelezi Rujewa, maji ni changamoto kubwa inayoukabili mji huo.” Hata wageni wengine wameona ni bora kuweka kambi katika mbuga za wanyama Ihefu kwa kuwa mji haujajitosheleza kihuduma,” alisema Nyenyembe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji.



No comments:

Post a Comment

Sponsor