Advertisement

Breaking

Friday, September 30, 2016

Utafiti Twaweza: Nchi Haiongozwi Kidikteta

Asilimia 58 ya Watanzania wamepinga kauli za baadhi ya wanasiasa kuwa Rais John Magufuli anaendesha nchi kidikteta huku asilimia 31 imesema haina uhakika na jambo hilo.

Aidha, imeelezwa kuwa asilimia 80 ya wananchi wanaona kwamba baada ya uchaguzi juhudi za kimaendeleo zipewe kipaumbele na vyama vya siasa.

Akitoa taarifa za utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Twaweza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze alisema ni asilimia 11 pekee ya Watanzania ndiyo waliosema nchi hii inaongozwa kidikteta.

“Baadhi ya wanasiasa na wasomi walitafsiri uongozi wa Rais Magufuli kama udikteta na neno hilo likawa mojawapo ya mambo yaliyounda Ukuta, asilimia 11 wanakubaliana na wazo hilo lakini asilimia 58 wanalipinga huku asilimia 31 wanasema hawana uhakika,” alisema Eyakuze.

Alisema kundi kubwa ambalo limejibu kuwa Rais Magufuli ni dikteta ni la vijana na watu matajiri na wenye uwezo wa juu kiuchumi kuliko masikini, wazee na watu wenye elimu ya chini; huku alisema asilimia 29 ya wananchi walio karibu ya vyama vya upinzani wanamuona Rais kuwa ni dikteta na asilimia tano ni wa chama tawala yaani CCM.

Aidha, alisema wananchi wana uelewa tofauti tofauti kuhusu neno udikteta, asilimia 32 walitafsiri kama kutawala kimabavu, asilimia 15 walitafsiri kuwa mtu mmoja ndiye mwenye maamuzi ya nchi nzima, huku asilimia 34 ya watu waliohojiwa hawaelewi maana ya neno hilo.

Katika demokrasia, Eyakuze alisema asilimia 51 ya Watanzania walisema mikutano inasaidia kuiwajibisha serikali huku asilimia 49 ikisema mikutano huvuruga umakini wa serikali na wananchi kudhoofisha shughuli za kimaendeleo.

Katika suala la maandamano, asilimia 50 walisema hawawezi kushiriki maandamano yoyote, asilimia 29 wanaweza kushiriki na asilimia 20 walijibu kuwa hawajui.

“Kati ya takwimu hizo, vijana waliosema wako tayari kushiriki maandamano yoyote na siyo lazima ya ukuta ni asilimia 35, watu wazima ni asilimia 15, wafuasi wa CCM asilimia 27 na wa vyama vya upinzani ni asilimia 43,” alisema Eyakuze.

Aidha alisema kuwa miongoni mwa waliosema kuwa hawatajiunga na maandamano asilimia 45 walisema ni kwa sababu wana wasiwasi itatokea vurugu na asilimia 29 walisema kwa sababu siyo njia sahihi za kutatua matatizo.

Alisema wananchi sita kati ya kumi waliunga mkono kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa wakiwemo wale wa vyama vya upinzani waliunga mkono suala hilo.

“Asilimia 60 waliunga mkono maamuzi ya Rais kuzuia mikutano ya kisiasa huku wazee wengi zaidi ndio walioonekana kuunga mkono zaidi uamuzi huo ambao ni asilimia 70 na vijana asilimia 55 na asilimia 31 ya wafuasi wa vyama vya upinzani wanakubaliana na kuzuiwa kwa maandamano ya Ukuta."

Asilimia 16 wananchi wanafahamu harakati za ukuta na asilimia 79 hawafahamu harakati hizo na miongoni mwa wanaofahamu uelewa wao kuhusu harakati hizo ni asilimia 48. Na kwamba kati ya wanaofahamu ukuta asilimia 50 walijibu wanaunga mkono ukuta na asilimia hamsini hawaungi mkono.

“Asilimia tisa kati ya wanaounga mkono ukuta katika maandamano ya Septemba mosi walipanga kushiriki ambapo ni pamoja na asilimia tatu ya wale wa chama tawala,” alisema.

Katika utafiti huo umeonesha kuwa wananchi hawakubaliani na mbinu zinazotumiwa na baadhi ya vyama vya upinzani katika kuhakikisha demokrasia inalindwa. 

No comments:

Post a Comment

Sponsor