Advertisement

Breaking

Saturday, October 29, 2016

Benk ya Twiga Bancorp Yafilisika....BoT Yachukua Usimamizi wake Kunusuru Amana za Wateja wa Benki Hiyo

Benki Kuu ya Tanzania imetangaza rasmi kuchukua usimamizi wa Benki ya Twiga Bancorp kuanzia jana kutokana na upungufu wa mtaji wa benki hiyo kiasi cha kuwa na deni la Shilingi Bilioni 21.

Benki Kuu pia imesimamisha shughuli zote za utoaji huduma za kibenki za benki hiyo kwa kipindi kinachokadiriwa kufikia wiki moja kuanzia jana tarehe 28/10/2016 ili kutoa nafasi kwa ajili ya kupanga taratibu za uendeshaji wa benki hiyo.

Maamuzi hayo yametangazwa jana jijini Dar es Salaam na Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndullu mbele ya waandishi wa habari, na kusema kuwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 56 (1)(g)(i) na 56(2) a-d cha taasisi za fedha ya mwaka 2006.

"Uamuzi huu umechukuliwa baada ya kubaini kuwa benki ya Twiga ina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu wa mtaji unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki ya Twiga kutaharisha usalama wa amana za wateja" Imesema sehemu ya taarifa ya Prof. Benno Ndullu.

Aidha, amewataka watu wote wanaodaiwa na benki hiyo kulipa madeni yao kupitia Benki Kuu ya Tanzania, na kwamba wadaiwa wote watafuatiliwa kokote waliko.

Mbali na maamuzi hayo, benki hiyo pia imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi na uongozi wa benki hiyo, huku ikimteua Meneja Msimamizi ambaye atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za benki hiyo kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya usimamizi wa benki hiyo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa usimamizi wa mabenki Bw. Keddedy Nyoni amesema benki hiyo ilianza na mtaji wa bilioni 7.5 lakini sasa ina deni la hadi bilioni 21.

No comments:

Post a Comment

Sponsor