Advertisement

Breaking

Wednesday, October 5, 2016

Bodi ya Wadhamni CUF Yawashitaki Mahakamani Profesa Ibrahm Lipumba na Msajili wa Vyama Jaji Francis Mutungi

Mgogoro  ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umeingia hatua ya pili baada ya Bodi ya Wadhamini kufungua kesi wakimtuhumu Prof. Ibrahim Lipumba, Jaji Francis Mutungi na watu 12 kwambwa, wanahujumu chama hicho.
 
Bodi hiyo jana imewasilisha maombi ya kufungua kesi katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam ya kuomba kibali cha kumzuia Jaji Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasas nchini kutofanya shughuli zake kinyume cha sheria.

Katika kesi hiyo, watuhumiwa ni pamoja na Prof. Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa chama hicho aliyerejeshwa kwa barua ya Jaji Mutungi na  watu 12 waliokuwa  wanachama  wa chama hicho.

Akizungumza na vyombo vya habari Juma Nassoro, wakili wa chama hicho alisema kuwa, wamewasilisha maombi hayo yaliyopelekwa kwa Eva Nkya, Msajili wa Mahakama hiyo ambapo ni ombi namba 75.

Wakili Nassoro alieleza kuwa, katika maombi ya awali waliyowasilisha kabla ya kesi ya msingi kuanza kusikilizwa  ni pamoja na mahakama kumuamuru Jaji Mutungi kutengua kauli yake ya uteuzi wa  Prof. Lipumba.

Alidai kuwa, mahakama hiyo iliwahi kubainisha kazi za msajili wa vyama ambapo sio kuingilia uamuzi wa ndani ya vyama vya siasa.

Wakili Nassoro alidai  kuwa, Jaji Mtungi hana mamlaka ya kutengua uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho .

Prof. Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na ujio wa Edward Lowassa ambaye baadaye aliteuliwa kuwa mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hata hivyo, mwaka huu aliaeleza kuandika barua ya kutengua barua yake ya wali ya kujiuzulu kwa madai ya kutaka kujenga chama jambo ambalo limesababisha chama hicho kupasuka.

Wiki iliyopita, Baraza Kuu la Uongozi la CUF, katika kikao cha dharura kilichofanyika Makao Makuu ya CUF, mjini Zanzibar lilimfukuza uanachama wa chama hicho Prof. Lipumba.

“Baraza Kuu linaweka bayana kwa wanachama wa CUF, Watanzania na mamlaka zote nchini kwamba kuanzia leo, Prof. Ibrahim Lipumba hana haki ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na shughuli zozote za chama,” ilieleza taarifa ya CUF.

Aidha taarifa hiyo ilidokeza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa baada ya baraza hilo kuridhika na mashtaka dhidi ya Prof. Lipumba kuongoza na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam tarehe 24 Septemba, 2016 mwaka huu.

“Baraza kuu limetumia uwezo wake, kwa mujibu wa Ibara ya 10 (1) (c) na kwa kura zote 43 za wajumbe wake waliohudhuria kumfukuza uanachama Prof. Ibrahim Lipumba,” ilieleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Sponsor