Advertisement

Breaking

Sunday, October 9, 2016

Majibu ya Daktari: Kijana Said Ally Aliyetobolewa Macho Na Scorpion Hawezi Kuona Tena

Na Dotto Mwaibale
MAJONZI na vilio vilitawala ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati Kijna Said Mrisho anayedaiwa kujeruhiwa na kutobolewa macho na Salumu Henjelewe maarufu kama Scorpion Buguruni Sheli alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mbele ya mkuu wa mkoa Dar es Salaam jana asubuhi kuwa hata ona tena katika maisha yake kufuatia kujeruhiwa vibaya kwenye mishipa ya macho na mtuhumiwa huyo na kupoteza uwezekano wa kuona.

"Nilijua ipo siku moja nitakufa lakini sikutegemea kuwa nitakuja kutolewa macho yangu kikatili kiasi hiki sijui mungu anampango gani na mimi wala sijui nini  hatima ya maisha yangu" alisema Mrisho ambapo ukumbi mzima uligubikwa na ukimya sanjari  na simanzi huku mke wake Stara Soud akishindwa kujizuia kulia.

Mrisho alisema anamshukuru sana Rais John Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa jitihada walizofanya za kumsaidia kupata matibabu lakini imeshindikana kwa kuwa mishipa yote yenye uwezo wa kumfanya aweze kuona imeharibiwa vibaya na mtuhumiwa huyo hivyo hataweza kuona tena katika maisha yake.
 
"Kama mishipa isingeharibiwa kwa visu mama yangu kipenzi Halima Lwiza Abdallah alikuwa yupo tayari kutoa jicho lake moja kwa ajili ya kunisaidia niweze kuona lakini kwa bahati mbaya hilo halitawezekana baada ya madaktari kunieleza kuwa mishipa ya macho yangu imeharibiwa" alisema Mrisho kwa huzuni na kuanza kulia.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema wamepokea kwa huzuni taarifa hiyo ya madaktari na kumuomba Mrisho asikate tamaa kwani serikali itaangalia jinsi ya kumsaidia.
 
Makonda alisema serikali itatoa sh.milioni 10 kama mtaji ili ziweze  kumsaidia wakati wakiangalia namna ya kuwashirikisha watu wengine kwa ajili ya kumsaidia.

Makonda alisema serikali itamsaidia kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa macho ya bandia ili awe katika mwonekano wa kawaida ingawa atakuwa haoni.

"Pamoja na kumpatia kiasi hicho cha fedha katika kipindi hiki cha mpito ambacho atakuwa akihitaji kwenda katika matibabu na sehemu zingine tutakuwa tukimsaidia usafari wa kwenda maeneo hayo"alisema Makonda.
Kijana Said Mrisho anayedaiwa kujeruhiwa na kutobolewa macho na Salumu Henjelewe maarufu kama Scorpion (kulia), akilia kwa uchungu wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana. Kushoto ni mke wake, Stara Soud
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiwa ameinama kwa uchungu wakati kijana huyo alipokuwa akizungumza na wanahabari.
 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Magembe (kushoto), akimfariji kijana Said Mrisho.

No comments:

Post a Comment

Sponsor