Advertisement

Breaking

Monday, October 17, 2016

Safari ya Tanzania ya viwanda yaanza......NBS Waagizwa kushirikiana na UNIDO na CTI kuvifanyia utafiti viwanda vidogo nchini

Serikali imeitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Viwanda Duniani (UNIDO) na Shirikisho la Viwanda Nchini (CTI) kuendelea kufanya utafiti ili kubaini idadi na maendeleo ya viwanda vidogo vilivyopo nchini.

Hayo yamesemwa jana  Jijini na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt Charles Mwijage wakati wa uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Uzalishaji bidhaa Viwandani mwaka 2013.

Dkt Mwijage alisema kuwa katika mataifa yanayoendelea duniani ikiwemo Korea Kusini, Malaysia na Singapore uchumi wa nchi hizo umeweza kukua kwa kiwango kwa juu zaidi kutokana na kuweka mkazo katika kuendeleza viwanda vidogo na vya kati.

Alisema katika kuharakisha kasi ya maendeleo ya viwanda vidogo  nchini, Wizara yake imekusudia kuwajengea hamasa Watanzania kupendelea kujenga viwanda vidogo vidogo na vya kati, kwani kukua kwa sekta ya viwanda nchini kutaisaidia kuinua uchumi wanchi.

“Asilimia 25- 40 ya mazao ya kilimo yanayovunwa huharibika kabla ya kufikishwa kiwandani, katika kukabiliana na hali hiyo Serikali imekusudia kujenga viwanda vidogo vidogo ili kuwawezesha wakulima wapate sehemu nzuri zaidi za kuhifadhi mazao yao” alisema Mwijage.

Aidha, Dkt Mwijage alisema, sekta ya viwanda vidogo vidogo nchini imeendelea kukua kwa kasi nchini ambapo hadi sasa kuna jumla ya viwanda 3800 vilivyoanzishwa nchini kuanzia Novemba 2015 hadi oktoba, 2016.

Katika hatua hiyo Dkt Mwijage alisema kuwa Wizara yake inaendelea kuhamasisha Sekta binafsi kuwekeza katika Sekta ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ikiwa jukumu kuu la Serikali ni kuhakikisha nchi inakuwa salama na inajenga mazingira wezeshi kwenye sekta binafsi kuzalisha na kufanya biashara.

Naye Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa matokeo hayo yanaonyesha mafanikio katika sekta ya viwanda ikiwemo kuongezeka kwa ajira zipatazo 264,223 nchini na kuchangia uchumi kwa takribani Shilingi bilioni 8.0 kwa mwaka 2013.

Alisema kuwa Takwimu za matokeo ya sensa ya uzalishaji viwandani ni rasmi na kuwataka watunga sera, wanasiasa, viongozi, sekta binafsi na watu binafsi kutumia  matokeo hayo kwa lengo la kuboresha Sekta ya viwanda nchini.

Na Beatrice Lyimo, MAELEZO

No comments:

Post a Comment

Sponsor