Advertisement

Breaking

Tuesday, October 25, 2016

Tanzania Yapata Mkopo Wenye Masharti Nafuu Wa Zaidi Ya Shilingi Bilioni 300 Kutoka Benki Ya Maendeleo Ya Afrika (Afdb) Na Serikali Ya Korea

Benny Mwaipaja, WFM, Seoul, Korea
TANZANIA, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Korea ya Kusini zimetiliana saini makubaliano ya pamoja kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya umeme gridi ya Kaskazini Magharibi inayoanzia mkoani Mbeya, Nyakanazi hadi Kigoma, yenye msongo wa kV 400 mbapo Serikali ya Korea imeahidi kutoa Dola za Marekani milioni 50 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 100.18, kwa ajili ya kugharamia mradi huo.
 
Hali kadhalika, Tanzania na Benki ya Exim ya Korea, zimesaini  Mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za marekani milioni 90.092 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 194 za Tanzania, kwa ajili ya mradi wa Upanuzi wa Miundombinu ya mfumo wa maji taka Jijini Dar es salaam.
 
Kwa upande wa Tanzania, Makubaliano pamoja na Mkataba vimesainiwa na Mhe. Dkt. Philip Mpango (MB) Waziri wa Fedha na Mipango kwa niaba ya Serikali, Oktoba 25, 2016 Jijini Seoul nchini Korea Kusini huku upande wa AfDB, aliye saini ni Rais wa Benki hiyo Adesina Akinwumi, na kwa upande wa Benki ya Exim, mkataba huo umesainiwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Benki hiyo Lee Duk-Hoon.
 
Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano na mkataba huo, Dkt. Mpango amesema makubaliano na mkataba vilivyosainiwa vina manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanzania.
 
“Wananchi wa Upande ule waanze kufurahia kwamba maendeleo yanakuja na hasa tunaposema maendeleo ya viwanda ambavyo ni lazima vitumie umeme, na kwamba mradi huu unatarajia kupelekwa hadi Mbeya” Amesisitiza Dkt. Mpango.
 
Dkt. Mpango, amesema kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa pia kwa kuwa serikali imedhamiria kuufungua ukanda wa Magharibi mwa Tanzania, kwa upande wa viwanda vya aina mbalimbali.
 
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uwekezaji) wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanzania-TANESCO, Decklan Mhaiki, amesema mradi wa umeme wa Nyakanazi hadi Kigoma utakuwa na urefu wa kilometa 280 na utakapo kamilika utaondoa changamoto ya shirika hilo kuzalisha umeme unatumika katika ukanda huo wa Magharibi hususan Kigoma, kwa kutumia majenereta ambayo uendeshaji wake ni ghali na umeme wake si wa uhakika.
 
“Kuleta laini kama hii, kwanza itapunguza gharama kubwa, na umeme wa ziada utakao zalishwa tunaweza kuuza nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, upande wa pili wa Ziwa Tanganyika, lakini kikubwa ni kuwahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwa na umeme wa uhakika” ameongeza Bw. Mhaiki.
 
Akizungumzia mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya maji taka Jijini Dar es salaam, Dkt. Philip Mpango, amebainisha kuwa mradi huo unatarajia kuwa na tija kwakuwa utatatua changamoto ya majitaka kutuama mitaani hasa wakati wa mvua na kusababisha magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu.
 
Akifafanua kuhusu mradi huo, Mchumi ambaye pia ni  Afisa anayeshughulika na utafutaji wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Melckzedek Mbise, amesema kuwa mradi wa maji wa Ruvu  unatarajia kuongeza wingi wa maji Jijini Dar es salaam, utakaosababisha uzalishaji wa maji taka pia kuongezeka, hivyo mradi huo wa kuondoa maji taka umekuja  wakati muafaka.
 
“Mradi huu umekuja wakati muhimu na mkopo una masharti nafuu sana” Amesisitiza Bw. Mbise.
 
Naye Afisa Mkuu wa utafutaji rasilimali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Sabra Issa Machano, amesema kuwa  kati ya nchi 54 za Kiafrika zinazohudhuria mkutano wa Tano wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Afrika, Mjini Seoul Korea, ni nchi nne tu zilizopewa mkopo na ufadhili ambazo ni Kenya, Uganda na Ethiopia, huku Tanzania ikipewa kiasi kikubwa zaidi cha fedha jambo linaloonesha kuwa Tanzania inakubalika Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Sponsor