Advertisement

Breaking

Tuesday, November 1, 2016

Jina la Paul Makonda latumika kutapeli wageni..... Jeshi la Polisi latoa tahadhari

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es-Salaam limetoa tahadhari kwa wakazi wa kanda hiyo pamoja na wageni kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam kwamba kuna baadhi ya matapeli wanatumia majina ya viongozi wa serikali kujipatia fedha kinyume na sheria za nchi.

Kamishna wa kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro  wakati akizungumza na waandishi wa habari jana alisema kuwa jeshi hilo hivi karibuni limepokea malalamiko kutoka kwa raia wa kigeni kuwa kuna wahalifu wanalitumia jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuwataka watoe fedha kwa madai ya kuwasaidia wanafunzi kupata vyuo nje ya nchi.

Alieleza kuwa, mnamo Oktoba mosi mwaka huu raia wa china Marco Li mfanyakazi wa kampuni ya Group six International alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Makonda na kumtaka atoe kiasi cha dola za kimarekani 3500.

Alisema tukio lingine lilitokea Oktoba 6, 2016 mkurugenzi wa kampuni hiyo Jensen Huang aliitumia fursa hiyo kumwomba mkuu wa mkoa huyo bandia kwamba amsaidie kumwidhinishia kuongezwa muda wake wa kuishi nchini ambao ulikuwa umeisha, na kwamba mhalifu huyo alimtaka atoe dola za kimarekani 7000 sawa na sh. Milioni 15.2.

Kamanda Sirro amewataka wakazi wote wa Dar es Salaam na wageni kuwa makini na matapeli hao na wakiona dalili za utapeli watoe taarifa katika vituo vya polisi kwa msaada zaidi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment

Sponsor