Advertisement

Breaking

Wednesday, November 9, 2016

Mtoto aliyepandikizwa betri moyoni afariki dunia

Mtoto Happiness Josephat (6) aliyefanyiwa upasuaji wa kupandikiza betri moyoni katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), amefariki dunia.

Mama mzazi wa Happiness, Elitruda Malley amesema Happiness alifariki dunia ghafla juzi mchana.

Alisema   Jumapili, mtoto huyo alikuwa mzima na walikwenda kanisani kutoa sadaka ya shukrani kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa mambo aliyowatendea na wakarudi nyumbani salama.

“Jana tumeamka vizuri lakini ghafla hali yake ilibadilika akaanza kulalamika kuwa anajisikia vibaya, tukamkimbizia Hospitali ya Selian hapa Arusha lakini tukiwa njiani alifariki dunia,” alisema.

Elitruda alisema kifo cha mwanawe kimemhuzunisha mno na  daima atamkumbuka.

“Alikuwa tayari amesharudi shuleni, alikuwa akiniambia kuwa atasoma kwa bidii ili ndoto yake ya kuwa daktari bingwa itimie aweze kusaidia watu wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali,” alisema.

Hata hivyo, alisema maziko ya Happiness yanatarajiwa kufanyika leo huko Mbulu mkoani Manyara.

Mkurugenzi wa JKCI, ambako Happiness alifanyiwa upasuaji, Profesa Mohamed Janabi amesema taarifa hiyo imemshtua ikizingatiwa mtoto huyo alikuwa anaendelea vizuri.

“Sikuwa na taarifa, nitawasiliana na mama yake   tujue hasa shida gani ilitokea, maana zipo sababu nyingi labda alipita jirani na mitambo ya umeme au simu, hizo ni sehemu hatarishi kwa mtu aliyewekewa betri kwenye moyo,” alisema.

Happiness alifanyiwa upasuaji huo wa historia nchini Julai 15, mwaka huu katika Taasisi ya JKCI wa kuwekewa betri maalumu kwenye moyo ambayo kitaalamu inaitwa ‘pacemaker’.

Kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibia mtoto huyo, wakati alipopekekwa hospitalini hapo, mapigo yake ya moyo yalikuwa 20.

Walisema  hali hiyo kwa mtoto si ya kawaida kwa vile  anapaswa kuwa na wastani wa mapigo 60 hadi 100 kwa umri wake.

Mtoto Happiness alizaliwa na tatizo hilo ambalo mara nyingi hali hiyo huwakumba watu wazima.

Moja ya ndoto za mtoto huyo ambayo alinukuliwa akiisema ni kuwa daktari bingwa wa kutibu magonjwa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Sponsor