Advertisement

Breaking

Wednesday, October 12, 2016

Nauli za daladala kuanza kulipwa kielektroniki kuanzia mwakani ili kubaini mapato halisi katika sekta hiyo

Mamlaka  ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetangaza kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ukataji wa tiketi za mabasi na daladala kwa njia ya kielektroniki.

Hatua hiyo ina lengo la kurahisisha upatikanaji wa mapato halali ya serikali pamoja na kuwafanya madereva na makondakta, kuajiriwa rasmi na wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri.

Pia mamlaka hiyo imezindua kampeni ya usafi kwa wafanyakazi wa daladala, ambayo inawataka kubadilisha sare za madereva na makondata, ambazo walishonewa na matajiri wao.

Sasa wafanyakazi hao watashona sare zao wao wenyewe ili wawe na uhalali wa kuzimiliki na kuzifanyia usafiri wa mara kwa mara.

Mkurugenzi wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema jana kuwa mfumo huo wa tiketi za daladala kwa njia ya elektroniki, utaanza kutumika Januari mwakani.

Lakini, aliongeza kuwa kuanzia Desemba mwaka huu, watafanya mpango huo kwa majaribio kwa mabasi yaendayo mikoani.

“Kwa sasa tumeanza mpango huo kwa majaribio kwa daladala za kampuni ya Christian, Desemba tutaenda kwa mabasi ya mikoani na Januari mwaka kesho, mfumo huo utaanza kwa mabasi na daladala zote,” alisema Kahatano.

Alitangaza mfumo huo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi kwa madereva, ambayo inahusisha usafi wa mwili, mavazi na mabasi uliofanyika katika stendi ya Makumbusho, Dar es Salaam. Katika kampeni hiyo, madereva na makondakta watajishonea wenyewe sare zao na sio wamiliki wa magari.

Kahatano alisema chini ya mfumo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki, utamfanya mmiliki wa basi kujua mapato yake halisi kwa siku na hivyo atawalipa wafanyakazi wake mshahara na Serikali itapata kiwango sahihi cha kodi. Kwa sasa ukataji wa tiketi za mabasi na ule wa daladala, unafanywa kwa tiketi zilizochapishwa.

Alisema kutokana na mfumo huo mpya, dereva haruhusiwi kumlipa mmiliki hesabu ya kila siku kama wanavyofanya sasa.

Badala yake, mmiliki ndiye atatakiwa kumlipa dereva na kondakta wa gari lake mshahara kila mwisho wa mwezi. Alisema ili malipo hayo yaweze kufanyika ni lazima madereva waajiriwe rasmi na walipwe chini ya mfumo wa ajira.

“Kwa hiyo dereva na mmiliki wataingia mkataba wa ajira tofauti na sasa hivi hakuna mkataba wowote kati ya tajiri na wafanyakazi wake, badala yake wanakubaliana tu kwamba hesabu ya siku ni kiasi fulani cha fedha na dereva anahangaika kukitafuta,” alisema Kahatano.

Kuhusu sare za madereva, alisema kwamba ndani ya wiki mbili madereva wa wilaya ya Kinondoni, wote wanatakiwa wawe wamebadili sare zao na kushona ambazo wamekubaliana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Awadhi Haji, alisema wao kama wasimamizi wa sheria, watahakikisha ndani ya wiki mbili madereva wote wa daladala wa wilaya ya Kinondoni, wanashona sare hizo mpya ambazo zimepitishwa na Sumatra.

Alisema kutokana na agizo hilo, hategemei kuwaona tena makondakta na madereva wachafu kwa kuwa watakuwa na sare zao binafsi ambazo watazitunza kuliko ilivyokuwa awali.

“Wale ambao watakaidi tutawakamata na kuwafikisha mahakamani.”

No comments:

Post a Comment

Sponsor