Advertisement

Breaking

Thursday, October 27, 2016

Rais Magufuli Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Mkurugenzi Mkuu Wa Mfuko Wa Maendeleo Wa Abu Dhabi Mohamed Al Suwaidi Ikulu Jijini Dar Es Salaam

Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais, Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan amemuahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo imedhamiria kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan ametoa ahadi hiyo kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi Bw. Mohamed Al Suwaidi aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli jana  tarehe 27 Oktoba 2016.

Mfuko wa maendeleo wa Abu Dhabi unashirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na katika mazungumzo ya leo Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo ameonesha nia ya kushirikiana zaidi na Tanzania katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli na barabara, usafiri wa anga na madini.

Pamoja kumshukuru Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Rais Magufuli ameialika nchi hiyo kupitia mfuko wake wa Maendeleo na wadau wengine wa maendeleo kuja kuwekeza hapa nchini katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa bandari, ujenzi wa viwanda, kilimo, uvuvi, gesi na kushirikiana katika ujenzi wa reli ya kati ambayo itazinufaisha nchi nyingine saba za Afrika Mashariki na kati ambazo hazina bandari.

“Tanzania imeamua kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na tayari katika bajeti yetu tumetenga Shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi, hivyo tunawakaribisha Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kushirikiana nasi, wapo wengi ambao wamejitokeza kushirikiana nasi lakini na nyie pia tunawakaribisha, mnaweza kuchukua sehemu ya reli na mkaijenga” alisema Rais Magufuli.

Aidha, Dkt. Magufuli aliutaka mfuko huo kufupisha muda unaotumika katika mchakato wa kuanza utekelezaji wa miradi ili kuharakisha matokeo yake na manufaa kwa wananchi.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

No comments:

Post a Comment

Sponsor