Advertisement

Breaking

Thursday, October 27, 2016

Wizara ya Afya imeyataja makundi yaliyoko hatarini kuambukizwa VVU nchini


October 27, 2016 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia kwa Waziri mwenye dhamana Ummy Mwalimu, imetoa tamko kuhusu huduma kwa makundi maalumu na yaliyoko hatari zaidi kuambukizwa na kuambukiza Virusi vya UKIMWI nchini Tanzania.
  
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kwa mujibu wa Takwimu za Viashiria vya UKIMWI na Malaria za mwaka 2011-2012, kiwango cha maambukizi ya VVU nchini kinakadiriwa kuwa ni asilimia 5.1 kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 – 49. Takwimu hizi pia zinaashiria kwamba, kwa kila watanzania 1000, watu 51 miongoni mwao wanaoishi na maambukizi ya VVU.

Inakadiriwa kuwa, kuna watu 1,400,000 wanaishi na VVU nchini Tanzania ambapo, watu 839,574 wanapatiwa tiba ya dawa za kupunguza makali ya VVU zinazotolewa katika vituo 4,000 vilikuwa vinatoa huduma hiyo nchi nzima hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu (2016).
 
Waziri Ummy amesema kutokana na mazingira ya Tanzania, imeonesha kuwa makundi maalumu ni makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukiza na kuambukizwa VVU, kwa kuzingatia takwimu za maambukizi ya VVU kwa makundi haya kuwa juu, huku Serikali ikiyataja makundi 13.
  • 1. Wasichana walio katika umri wa balehe walio katika mazingira hatarishi.
    2. Vijana walio katika umri wa balehe.
    3. Watoto yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi (yaani watoto wanaoishi mitaani).
    4. Wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao.
    5. Wanawake wanaofanya ngono kinyume na maumbile.
    6. Watu wanaotumia dawa za kulevya hasa wale wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano.
    7. Wanawake wanaofanya biashara ya ngono na wateja wao.
    8. Wafungwa.
    9. Wakimbizi na wafanyakazi wanao hamahama hasa madereva wa malori ya masafa marefu.
    10. Wachimba madini na jamii zilizopo katika maeneo ya migodi.
    11. Wavuvi na jamii zilizopo katika maeneo ya uvuvi.
    12. Wafanyakazi wa kwenye mashamba makubwa.
    13. Wajenzi wa barabara  na watu wenye ulemevu.
Kuna ushahidi wa kipiedemilojia kwa programu za VVU na UKIMWI kulenga makundi maalum. Katika nchi zilizo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, vijana balehe wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 35 ya maambukizi mapya ya VVU. 
 
Aidha, kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU nchini Tanzania, kinaonekana miongoni mwa makundi maalum (asilimia 26 miongoni mwa Wanawake wanaofanya Biashara ya Ngono, asilimia 36 miongoni mwa wanaotumia madawa ya kulevya kwa kujidunga sindano na asilimia 25 miongoni mwa wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao).

No comments:

Post a Comment

Sponsor