Advertisement

Breaking

Thursday, October 6, 2016

Serikali Yachachamaa....Walimu Waliomfanyia Ukatili Mwanafunzi Watimuliwa Chuoni, Mkuu wa Shule Apoteza Kibarua

Mitandao ya kijamii imeendelea kuzua balaa baada ya kuibua tukio la walimu watano wa Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya wakimshambulia mwanafunzi kwa fimbo, makofi, ngumi na mateke, vitendo vilivyosababisha mawaziri watatu kuchukua hatua dhidi yao.

Mkanda huo ulisambaa jana, ikiwa ni siku moja baada ya Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar kumtimua kazi askari wa usalama barabarani kwa kosa la kuomba rushwa baada ya tukio hilo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki.

Tukio la walimu kumshambulia mwanafunzi huyo limesababisha mawaziri watatu-Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani), Joyce Ndalichako (Elimu) na George Simbachawene (Tamisemi)-kuchukua hatua kila mmoja kwenye eneo lake.

Video hiyo inaonyesha walimu hao wakimkamata mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu anayejulikana kwa jina la Sebastian Chinguku, kumuangusha chini na baadaye kuanza kumshambulia kwa fimbo, makofi, ngumi na mateke, huku mmoja akionekana kutanua mikono yake ili aweze kumpiga vizuri kichwani.

Wakati wakimshambulia, sauti za kike zinasikika zikiwataka walimu hao waache kumpiga mwanafunzi huyo, huku moja ya kiume ikiwataka wenzake wamuweke vizuri ili apige.

Habari kutoka kwa watu mbalimbali zinasema sababu ya walimu hao kufanya kitendo hicho ni madai kuwa mwanafunzi huyo alionyesha kiburi kwa kugomea adhabu.

Mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu  alisema tukio hilo lilitokea Septemba 28 saa 3:00 asubuhi wakati mwalimu anayeitwa Frank Msigwa alipotaka kujua sababu za baadhi ya wanafunzi kutofanya zoezi la somo la Kiingereza alilotoa siku mbili kabla ya tukio.

“Mwalimu Frank alisema wote ambao hawakufanya kazi yake aliyowapa Jumatatu wapite mbele na watachapwa viboko vitano, vitano na wote tulipita. Lakini Sebastian alimweleza mwalimu kuwa siku hiyo (waliyopewa kazi) hakufika shuleni kwani alikuwa anaumwa mkono na mguu,” alisema mwanafunzi hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe.

Alisema mwalimu huyo hakukubali maelezo ya Sebastian na kusisitiza lazima aadhibiwe na ndipo mwanafunzi huyo akachukua begi la madaftari ili aondoke.

“Alipochukua begi mwalimu, alimkunja shati na kumuuliza anafanya nini. Sebastian akamjibu kuwa anataka kwenda nyumbani kwa kuwa hawezi kuchapwa kutokana na kuumwa mkono na mguu na ndipo mabishano yalipoanza na mwalimu akawaita wenzake watano wakaja darasani na kuanza kumshambulia kwa kumpiga fimbo,” alisema na kuongeza;

“Mwalimu alinituma mimi nikachukue fimbo nyingine kwa ajili ya kumchapia Sebastian, wakati narudi nikakuta wanamburuza kutoka darasani kwenda ofisini huku wakim piga.”

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alisema kilichosababisha hayo kutokea ni mwanafunzi huyo kukataa adhabu tatu alizopewa, ambazo ni kupiga push-up, kupiga magoti au kuchapwa viboko viwili.

“Alianza kwa kuwapa adhabu ya push-up, lakini Sebastian akakataa akisema anaumwa goti. Baadaye akamwambia apige magoti, lakini pia akakataa akisema anaumwa goti na baadaye akamwambia apigwe viboko viwili, lakini pia akakataa.” alisema Makalla.

Makalla alisema baada ya kuigomea adhabu hiyo, mwalimu Msigwa na wenzake wawili, John Deo na Sanke Gwamaka, walimpeleka ofisini ambako walimshambulia kama inavyoonekana kwenye video.

“Baada ya tukio hilo waalimu hao walitoweka shuleni hapo. Wakati wanamshambulia mwanafunzi huyo, kulikuwepo na mwalimu mwingine aliyewasihi wasiendelee kumpiga kijana huyo na ndiye aliyerekodi tukio hilo,” alisema.

Mwalimu ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema baada ya tukio hilo, walimu hao walikwenda polisi kushtaki kuwa wameshambuliwa na mwanafunzi huyo.

“Hatujui walikwenda kituo gani cha polisi kutoa taarifa hiyo kuwa wameshambuliwa, lakini kilichokuwa kimepangwa ni hicho,”alisema. 

Tukio hilo lilisababisha vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa kufika shuleni hapo na kumuweka kitimoto mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule na wenzake watatu ambao walikwenda kutoa maelezo polisi.

Baadaye jana, Waziri Mwigulu aliliagiza Jeshi la Polisi kufuatilia tukio hilo, wakati mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi aliwataka polisi kuchunguza tukio hilo na kutoa majibu kuhusu nini kilichotokea.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako alitangaza kuwatimua vyuoni walimu hao, akisema kwa mujibu wa taratibu za vyuo vikuu, kitendo hicho ni kosa la jinai na hivyo haliwezi kufumbiwa macho.

Alisisitiza kuwa shambulio lililofanywa na walimu hao ni la kikatili na linakwenda kinyume na taaluma ya ualimu hivyo hawafai kuendelea nayo.

Tukio hilo pia liligusa wizara ya Simbachawene, ambaye alitangaza kumshusha cheo mwalimu mkuu kwa kufumbia macho kitendo hicho na kutotoa taarifa mpaka video ilipozagaa kwenye mitandao ya kijami.

“Kutochukua hatua ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kunaonyesha kulikuwa na dalili ya kulificha suala hili,” inasema taarifa ya Simbachawene kwa vyombo vya habari.

Sambamba na hilo Simbachawene ameviagiza vyombo vya usalama kuwatafuta walimu hao na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Dhahiri Kidavashari aliwataja walimu hao kuwa ni Frank Msigwa na John Deo wote kutoka Chuo Kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Duce) na Sanke Gwamaka wa Chuo cha Ualimu cha Mwalimu Nyerere. Majina ya wengine wawili hayakupatikana.

Kamanda Kidavashari alisema kwamba kwa hatua za awali tayari wanamshikilia mkuu wa shule hiyo kwa ajili ya mahojiano zaidi.

“Kuna vitu vingi ambavyo tunahitaji kupata hapa shuleni, pamoja na kumshikilia mkuu wa shule, pia tumewachukua baadhi ya walimu na wanafunzi kwa ajili ya mahojiano ili waweze kutusaidia katika suala hili na wahusika lazima wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema.

Akizungumza shuleni hapo katibu tawala wa mkoa, Mariam Mtunguja alisema kitendo cha walimu hao ni cha kinyama na hakipaswi kufumbiwa macho na kwamba uchunguzi unaendelea ili kuwabaini wahusika wote.

“Kama serikali ya mkoa tunalifuatilia suala hili kwa karibu ikiwa ni pamoja na kumtafuta huyo mtoto nyumbani kwake kujua hali yake ilivyo kwani tunavyosikia ni kwamba hajafika shuleni kutokana na kipigo hicho,” alisema.

Baba wa mwanafunzi huyo, John Chinguku ambaye ni mfanyakazi wa benki ya NMB Tawi la Mbozi mkoani Songwe, amesema mtoto wake anatibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akiuguzwa na mama yake.

Alisema aliona video ikimwonyesha mtoto wake akipigwa sana na walimu na baadaye kupigiwa simu na fundi anayejenga nyumbani kwake eneo la Uyole, ambaye alimtaarifu kuwa polisi walifika nyumbani hapo kumchukua mtoto ili akatoe maelezo ya kupigwa na mwalimu.

 Alisema baada ya kuiona video alishindwa kufanya kazi na kufanya taratibu za kupata ruhusa kurudi Mbeya ili aweze kusimamia matibabu ya mtoto wake.

Kuhusu kutimuliwa kwa wanachuo hao, Rais wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso), Erasmi Leon alisema bado wanaendelea kuchunguza ili kubaini kama kweli walimu hao ni wanafunzi wa UDSM.

Kuhusu uamuzi wa waziri, alisema: “Hakuna utetezi wowote ambao (walimu) wanaweza kutoa kujilinda dhidi ya kitendo kile cha kinyama. Alichokifanya waziri ni sawa kabisa ila ingekuwa busara angetoa maelekezo kwa vyuo halafu baadaye akafuata mrejesho.”

No comments:

Post a Comment

Sponsor