Advertisement

Breaking

Tuesday, October 11, 2016

Utafiti wadai mtu mmoja kati ya wanne ni kichaa, Wizara yaeleza sababu


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu amesema utafiti unaonesha kuwa kwa kila watu wanne duniani, mmoja ana matatizo ya afya ya akili.

Alisema hayo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani yaliyofanyika kitaifa Dar es Salaam chini ya kaulimbiu: “Utu katika Afya ya Akili, Huduma za Kisaikolojia na Afya ya Akili kuwa Huduma ya Kwanza kwa Wote”.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy wananchi wanapaswa kuwa makini kuchunguza afya zao za akili kwa sababu utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaashiria kuwa jamii kwa sasa inakumbwa na maradhi mengi ya namna hiyo.

“Takwimu kwamba kila watu wanne, mmoja wao ana ugonjwa wa akili ni kielelezo tosha kwamba ipo haja ya jamii kujitambua na kuona umuhimu wa kupewa elimu ya afya ya akili na kisaikolojia,” alisema na kufafanua:

“Magonjwa ya akili ni yanayoathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, hivyo kuwa na tabia au mwenendo ulio tofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, desturi na nyanja nyingine za kijamii.”

Aliongeza: “Tunapaswa kukumbuka kuwa hakuna afya njema ya kimwili kama hakuna afya ya akili; na pia nchi yetu ikiwa na wananchi wenye afya bora ya akili ni hazina kubwa kwa Taifa.”

Ummy alibainisha: “Miongoni mwa watu wanaopata matatizo ya kiakili ni wachache tu ambao wanaweza kufikia na kupata huduma ya afya ya akili, hata hao wanaohudhuria vituo vya afya, ni wachache wamekuwa wakipata huduma stahiki.

“Katika nchi yetu tumekuwa tukikabiliwa na matatizo kama hayo kutokana na ufinyu wa bajeti, ukosefu wa wataalamu katika vituo vya kutolea huduma, ukosefu wa vifaatiba na dawa kwa wagonjwa wenye matatizo ya akili, kijamii na kisaikolojia.”

Waziri Ummy alisema hali hiyo inatokana na matatizo yanayoikabili jamii yakiwamo majanga yanayoiandama dunia.

Mwalimu alitoa mfano kwamba, mwaka jana Tanzania ilionesha kuwa na wagonjwa wa afya ya akili 311,789 kulingana na takwimu za waliokwenda hospitali kuchunguzwa.

 Alibainisha kwamba hali hiyo inaashiria kuwa idadi hiyo ni kubwa zaidi, kwa sababu kuna ambao wana matatizo hayo lakini hawaendi hospitali au wamekuwa wakienda kupata huduma tofauti.

Alisisitiza kuwa katika kukabaliana na ukweli huo, jitihada zimefanywa na serikali kutoa huduma za afya ya akili na saikolojia.

Mwalimu alisema Serikali itaendelea kuongeza juhudi katika kutoa huduma na elimu ya afya ya akili kuanzia ngazi ya msingi na kuwa na kitengo maalumu kinachotoa huduma hizo katika hospitali zote nchini.

Hatua nyingine alisema ni kuboresha upatikanaji wa dawa za kutibu magonjwa ya akili katika hospitali zote za Serikali.

Aliongeza kuwa Serikali imeimarisha matibabu ya akili na saikolojia katika hospitali za mikoa na rufaa hii ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa afya ya akili wakiwamo madaktari bingwa na wauguzi ili kuboresha huduma kwa wagonjwa wa nje na waliolazwa.

Alifafanua kuwa sababu za kijamii zinazoweza kusababisha mtu kupata magonjwa ya akili ni umasikini uliokithiri, kutengwa na kubaguliwa na jamii. Sababu zingine alizitaja kuwa ni kunyanyaswa kimwili na kingono, kuwa tegemezi, kupoteza mali, kazi, ulevi, kukosa huduma muhimu na unyanyapaa.

Aliiasa jamii kuachana na Imani potofu kuwa chanzo cha ukichaa ni ushirikina na hivyo kupoteza fedha na mali nyingi kwa waganga wa kienyeji wasio waaminifu.
==

No comments:

Post a Comment

Sponsor