WAKATI jamii ikiendelea kulaani kupigwa kikatili mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Kutwa ya Mbeya, Sebastian Chinguku, mwezi uliopita, imeelezwa kuwa wanafunzi wengi wamekosa nidhamu na wamejengewa kiburi na wazazi na walezi wao kudharau na kudhani wako juu ya walimu.
Walimu wamesema pamoja na kwamba kitendo alichofanyiwa mwanafunzi Chinguku ni cha kikatili na kisichokubalika, lakini wengi wao hudhalilishwa na wanafunzi mbele ya wenzao, na wanapopewa adhabu, hutetewa na walezi na wazazi wao, jambo linalowaongezea kiburi na kutobadilika.
Baadhi ya wazazi na walezi, wamekiri kutotekeleza ipasavyo wajibu wa kulea, ingawa wametupia lawama maendeleo ya teknolojia na makundi mabaya, kuchangia huwaharibu watoto wao huku wanafunzi wakieleza wazi kuwa nidhamu yao inahitaji kupigwa msasa.
Walimu, wazazi na wanafunzi, kwa nyakati tofauti wakizungumza na gazeti hili, mara baada ya kutokea kwa tukio la Mbeya Day, walisema suala la maadili na miongozo ya adhabu pamoja na uhusiano kati ya mwanafunzi, mwalimu na mzazi, linapaswa kuangaliwa upya. Kauli hiyo pia ilitolewa na viongozi mbalimbali wa serikali.
Walimu wazungumza Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mchanganyiko ya Kariakoo, Dar e Salaam, Adella Tukay, alisema haikuwa sawa kwa mwanafunzi wa Mbeya kupewa adhabu kali namna ile, lakini kosa la mwanafunzi huyo kugoma kufanya kazi aliyopewa na mwalimu wake ni la unyanyasaji na udhalilishaji kwa mwalimu, tena la kufedhehesha.
“Mimi nimewahi kukutana na udhalilishaji wa wanafunzi kwangu, si mara moja, tena makubwa zaidi ya huyo mwanafunzi na nilitoa adhabu. Kuna adhabu unaweza kumpa mwanafunzi kutokana na kosa lake,” alisema Tukay.
Alisema yeye akikutana na mwanafunzi mlevi, mvuta bangi au anajihusisha na mapenzi, hujenga ukaribu naye ili kujua sababu ya mwanafunzi kuwa alivyo kabla ya kutoa adhabu na baada ya hatua hiyo, mwanafunzi asipobadilika kwa kipindi kirefu, humpa muda wa kupumzika nyumbani na ikibidi, hufika nyumbani kuona mazingira anayoishi.
“Ila ukweli ni kwamba ualimu unahitaji moyo na uvumilivu mkubwa kwa kuwa wanafunzi huwapandisha hasira walimu kila sekunde. kumchapa mwanafunzi viboko inaruhusiwa ila si vibao, yule wa Mbeya (Mbeya Day) alivuka mipaka. Kikubwa kabla hujaingia shuleni, mwalimu lazima umuombe Mungu akupe busara na hekima siku hiyo, maana ni kazi kukabiliana na hiki kizazi cha nyoka (watoto watukutu), ila kupitia sala na ukimtegemea Mungu utaweza pia kuwasaidia wanafunzi kuwa na nidhamu,” alisema Tukay.
Mwalimu wa Shule ya Msingi, Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam, Teodora Puka alisema kipigo kile si sahihi, ingawa wanafunzi wenyewe wanachangia kuchochea hasira walimu. Alisema kitendo cha mwanafunzi kugomea adhabu, ambayo wengine wamefanya, kinaonesha yupo juu ya mwalimu.
“Hii inatia hasira maana mwanafunzi mwingine anakupiga kofi mbele ya wanafunzi wenzake, anakwambia utanifanya nini,” kweli nidhamu kwa wanafunzi imeshuka na inachangiwa na wazazi pia kutotekeleza wajibu wao na baadhi ya walimu pia kutokujua misingi ya ualimu,” alisema Puka.
Puka alishauri walimu na mtu yeyote kutokufanya uamuzi akiwa na hasira au ana furaha sana, alishauri pia miongozo ya ualimu izingatiwe.
“Jambo lolote ukiamua ukiwa katika hali hizi, unaweza kuja kujuta baadaye,” alisema Puka.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mjimpya, Lukobe, Morogoro, Magreth Raymond alisema nidhamu kwa wanafunzi imeshuka na ukaribu baina ya walimu na wanafunzi umepungua. Alisema amewahi kukutana na wanafunzi wakorofi, tena wenye ukorofi sugu na mara zote huwakabidhi kwa viongozi wa juu wa shule ili wawachukulie hatua zaidi.
Alishauri pia walimu wafuatilie maisha ya wanafunzi mpaka nyumbani, kwa kuwa malezi ya nyumbani yanachangia mtoto kuwa mtukutu kupitiliza.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Nelson Mandela, Morogoro, Veronica Mshare, alisema suala la kuzuia hasira kwa walimu ni la muhimu ili kudhibiti kutoa adhabu isiyomrekebisha mwanafunzi. Hata hivyo, alisema serikali imechukua uamuzi wa haraka kuhukumu walimu bila kuuliza chanzo wakati wanafunzi watukutu ni wengi.
Wazazi watoa neno
Baadhi ya wazazi jijini Dar es Salaam, waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa gazetini, walikiri kutotekeleza wajibu wao katika malezi na kudai baadhi yao huacha dunia iwafunze watoto na hivyo kutengeneza kizazi cha uharibifu, jambo walilosema ni hatari kwa jamii na taifa zima.
“Mtoto anakwenda shule, mzazi huulizi maendeleo yake, hujui tabia zake, marafiki zake wala hujishughulishi na chochote, sasa hapa unamlaumu mwalimu kivipi? Watoto wetu wenyewe hawana adabu, lazima wazazi tubadilike katika kutoa malezi,” alisema mzazi wa mwanafunzi wa shule ya sekondari Mshikamano, Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Mzazi mwingine, Hamida Mustafa, mkazi wa Goba, Dar es Salaam alisema lawama wanapaswa kutupiwa wazazi, kwa kuwa wamekosa muda wa kukaa na watoto na kutoa malezi mazuri na kuwabebesha walimu kila kitu.
Mkazi wa Kibangu, Hamis Suleiman mwenye mtoto wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Kibasila, Dar es Salaam, alisema malezi kwa watoto hivi sasa, yanahitaji ukaribu zaidi kwa kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia, yanachangia kuwaharibu watoto kama wazazi hawatawafuatilia kwa karibu.
Mkazi wa Sinza, Jenifa Shija ambaye mwanawe anasoma darasa la nne, alisema wazazi wengi wamekuwa na shughuli nyingi na kusahau kuwajenga kinidhamu watoto wao hivyo wazazi wanapaswa kujirudi na kumwomba Mungu awawezeshe kuwalea watoto vizuri. Wanafunzi watoa ufumbuzi Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na gazeti hili walisema mahusiano chanya baina ya walimu na wanafunzi ni suluhu ya kurejesha nidhamu na maadili kwa wanafunzi na walimu.
Mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Michael wa Mbezi High, Dar es Salaam, alisema baadhi ya walimu wamekosa haiba ya ualimu, wanajenga uhusiano mbaya na wanafunzi na wanaogopa kuwa nao karibu na kusababisha kutokujua tabia za wanafunzi. Kwa upande wake, mwanafunzi wa shule ya sekondari Benjamin Mkapa, Michael Lucas alisema nidhamu kwa wanafunzi inapaswa kupigwa msasa wa nguvu kwa kuwa, pamoja na kwamba wapo walimu wasiozingatia miiko na misingi ya kazi yao, wanafunzi wamekuwa jeuri na wameota pembe mpaka wanawatishia maisha walimu. “Kuna mazingira walimu wanateseka, tunakosa kumheshimu mtu anayekutoa katika ujinga utamheshimu nani? Nadhani ipo haja ya kuweka mkazo wa nidhamu kwa nguvu ya ziada kwa wanafunzi, hali ni mbaya huku mashuleni,” alisema Lucas. Naye mwanafunzi wa shule ya msingi Minazi Mirefu iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam, Khadija Mbaga alisema hakuna walimu wanaotumia waraka wa elimu katika kutoa adhabu hasa ya viboko kwani huchapwa visivyo na idadi. Alisema tena wanafunzi wa kike wamekuwa wakichapwa na walimu wa kiume huku mara nyingi walimu hawana mahusiano mema nao kiasi ambacho huwaogopa hata kuwaomba ushauri kwa masuala mbalimbali ya kijamii pale wanapokabiliana nayo. Mwanafunzi wa Shule ya sekondari Kitunda, David Nyang’ombe yeye alisema kwamba mahusiano kati ya walimu na wanafunzi sio mabaya, na adhabu ya fimbo kwa mwanafunzi ipo shuleni kwake. “Mimi niliwahi kuchapwa fimbo nne, lakini kuna mwanafunzi nilishuhudia akichapwa hadi fimbo 10, idadi ya fimbo inategemea na mwalimu mwenyewe,” alisema mwanafunzi huyo lakini alisisitiza adhabu kuwa suala la mwisho kwa mwanafunzi. Juma Mang’ara ambaye anasoma shule ya sekondari ya Nyerere iliyoko mkoani Mbeya, alisema kwamba mahusiano kati ya mwalimu na mwanafunzi ni ya kibabe na hakuna urafiki kati ya mwalimu na mwanafunzi. “Mwanafunzi kuchapwa ni jambo la kawaida, idadi ya viboko inategemea na mwalimu anayekupa adhabu,” alisema Juma.
No comments:
Post a Comment