Mhasibu
wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Hamida Masoli amefikishwa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupandishwa kizimbani akikabiliwa
na mashtaka 95, yakiwamo ya uhujumu uchumi, ubadhirifu, wizi na
kusababisha hasara ya zaidi ya Sh71.7 milioni.
Mwendesha
mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Denis
Lekayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage amedai mshtakiwa
anakabiliwa na shtaka moja la ubadhirifu na ufujaji, shtaka moja la
kusababisha hasara, mashtaka 44 ya kutumia ofisi vibaya na kumdanganya
mwajiri wake na mashtaka 49 ya wizi.
Lekayo
amesema kati ya Julai Mosi, 2007 na Desemba 31, 2011 kwenye ofisi za
Makao Makuu ya TTCL yaliyopo wilayani Ilala, Masoli akiwa mwajiriwa
alifuja Sh70,469,407 kwa matumizi yake binafsi. Alidai kati ya Mei 2007
na Novemba 30, 2011 kwenye ofisi za TTCL kwa makusudi mshtakiwa
alisababisha hasara kwa Serikali ya Sh71,769,407.
Masoli
anadaiwa kati ya Septemba 24 na 30, 2007, kwa nafasi yake ya mhasibu
wa mishahara TTCL, alitumia nyaraka ya uongo kumdanganya mwajiri wake
akijaribu kuonyesha Sh567,261,684 zilitumika kwa mishahara ya kampuni
hiyo wakati akijua ni uongo.
Mshtakiwa
anadaiwa kwa nafasi yake kati ya Mei 15 na 30, 2007 aliibia kampuni ya
TTCL fedha hizo ambazo alikabidhiwa kwa mujibu wa sheria.
Baada
ya kumsomea mashtaka, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi
unaendelea na kwa kuwa mashtaka yameunganishwa na uhujumu uchumi na kwa
mujibu wa hati iliyowasilishwa mahakamani na Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP), Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayo mamlaka ya kusikiliza
maombi ya dhamana.
Hakimu
Mwijage alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao
kila mmoja atasaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh20 milioni pia, awe
na barua kutoka kwa mwajiri wake. Mshtakiwa ametakiwa kuwasilisha hati
yake ya kusafiria Takukuru ndani ya siku saba na katika muda huo
asipofanya hivyo atafutiwa dhamana.
Mshtakiwa alikamilisha masharti ya dhamana na kuachiwa huru. Kesi imeahirishwa hadi Novemba 8, 2016 kwa ajili ya kutajwa.
No comments:
Post a Comment