Advertisement

Breaking

Wednesday, October 12, 2016

UVCCM Wamtembelea Majeruhi Aliyetobolewa Macho na Scorpion.....Wataka Jeshi la Polisi Liyabane Majambazi

UMOJA wa Vjana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umelihimiza Jeshi la polisi nchini kutambua kuwa ujambazi, wizi wa kutumia silaha na uporaji bado ni tatizo linalohitaji kushughulikiwa kwa nguvu zote kama ambavyo nchi ilisimama na kutekeleza operesheni mbalimbali za ukombozi.

Pia, umesisitiza kuwa usalama wa raia na mali zao unahitaji kulindwa ili kuepusha vifo, hasara, unyang’anyi wa mali na vilema vya maisha kutokana na matukio yanayoweza kuwakumba wasio na hatia mijini na vijijini.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alieleza hayo jana alipomtembelea kumjulia hali majeruhi Said Ally, Mabibo Hostel.

Saidi alijeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake ikiwa ni pamoja na kutobolewa macho katika tukio wizi wa kutumia silaha Buguruni mjini Dar es Salaam, Septemba mwaka huu.

Shaka alisema tatizo la uhalifu, unyang’anyi, uporaji na ukwapuaji mali kwa kutumia nguvu na silaha, linahiaji kutazamwa kwa kina na upana unaostahili na vyombo vyenye dhamana vinavyosimamia usalama wa raia na mali zao.

Alisema kuna haja ya polisi kubuni mbinu mpya za kukabiliana na makundi ya wezi, waporaji na majambazi kabla hawajaleta madhara na hasara kama ilivyomtokea Said ambaye sasa  amesababishiwa ulemavu wa kudumu wa kutoona.

“Kila siku mbinu za uhalifu, ujambazi, wizi wa kutumia nguvu na silaha hubadilika, jukumu la kupambana na matukio hayo hatari ni la polisi kwa kushirikiana na raia wema, janga hili likiachwa wananchi wataishi kwa mashaka na hawatajituma kujiletea maendeleo,”alisema Shaka.

Alisema ikiwa wananchi wanajituma kwa bidii kutafuta fedha na kubuni miradi ya kiuchumi halafu majambazi na wanyang’anyi wanapora na kumfilisi aliyetafuta ndani ya saa chache, hilo linaweza kuwatia hofu mwananchi na wajasiriamali na kuwafanya washindwe kujituma kikamilifu jambo ambalo litakuwa na madhara makubwa katika kuzalisha mali na kukuza uchumi.

Akizungumza kwa masikitiko na huzuni kubwa , Shaka alisema tamaa ya kupata utajiri kwa njia haramu kwa mtu mmoja mmoja au kikundi, kumemsibaishia hasara ya maisha dhidi ya Said ambaye kwa sasa amekoseshwa uwezo wa kuendelea kupiginia maendeleo yake ya kiuchumi na taifa kwa ujumla.

“Ifike mahali tatizo la uhalifu, ujambazi na uporaji lishughulikwe kama harakati za mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi, ukoma na kifua kikuu, tukilipuuza tatizo hili litaigharimu jamii na kuwaletea kadhia ya umasikini wananchi na Tanzania kwa ujumla,”alieleza.

Kwa upande wake majeruhi Said aliishukuru UVCCM kwa kuonyesha kumjali na kufika kumjulia hali kutokana na janga lililomkuta na kumpa msaada huku akiwahimiza waendelee kuikumbusha serikali isimuache kwa sababu amedhulumiwa utu wake na watu aliowatuhumu kuwa ni majambazi bila ya hatia wala kosa lolote.

Said alisifu ujio huo wa ujumbe kutoka Makao Makuu ya UVCCM Taifa ulioongozwa na Shaka, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam Omar Matulanga na makatibu wa umoja huo kutoka wilaya tano za mkoa huo.

Alisema akiwa kijana amefarijika kutembelewa na vijana wenzake huku akiwahimiza wasimchoke kwa sababu sasa amekuwa kipofu na hajimudu tena kimaisha.

“Endeleeni kuikumbusha serikali yetu na wasamaria wema wasinisahau, nina nguvu, akili na maarifa ya kujituma ili nizalishe ila nimedhulumiwa macho yangu na sina hakika kama nitaona kama mwanzoni “alisema

No comments:

Post a Comment

Sponsor