Advertisement

Breaking

Sunday, September 18, 2016

Mikoa kumi hatarini kupigwa na tetemeko

WAKATI Taifa likijikusanya kusaidia walioathirika kwa tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi iliyopita mkoani Kagera, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), umetaja mikoa kumi iliyo hatarini kukumbwa na janga hilo wakati wowote.

Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Profesa Abdulkarim Mruma amesema kuwa matetemeko ya ardhi Tanzania ni jambo la kawaida kutokea kwa sababu nchi imepitiwa na Bonde la Ufa lenye vitovu vya matetemeko.

“Tetemeko si jambo la bahati mbaya kwa sababu kitaalamu hali hiyo inaweza kutokea wakati wowote katika nchi zilizopitiwa na bonde hilo,” alisema Profesa Mruma.

Kuonesha uhalisia wa uwezekano wa kutokea matetemeko zaidi nchini, Profesa Mruma alisema tetemeko hilo la Kagera ni la pili kutokea mwaka huu, ambapo miezi miwili iliyopita lilitokea lingine mkoani Dodoma lililokuwa na uzito wa skeli ya Richter 5.1.

Mikoa ya Pwani

Katika Jiji la Dar es Salaam, Profesa Mruma alisema eneo la Bonde la Mto Ruvu linaloanzia Mkoa wa Pwani hadi katika jiji hilo na katika bonde la Mto Mzinga, unaopita maeneo ya Mbagala, kuna kitovu cha tetemeko la ardhi, hivyo kuwa katika hatari ya kutokea wakati wowote.

Profesa Mruma alisema Katika Ukanda huo wa Pwani, kitovu kingine cha tetemeko la ardhi kiko katika fukwe za Bahari ya Hindi hasa katika Mkoa wa Mtwara, kwenye makutano ya bahari hiyo na nchi ya Madagascar.

“Mkoa huu (Dar es Salaam) pamoja na maeneo yote yaliyo katika Ukanda wa Bahari hayako salama kwani pia yanaweza kutokewa na matetemeko ya ardhi,” alisema.

Mkuu wa Idara ya Jiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Elisante Mshiu, yeye  alisema Jiji la Dar es Salam haliko salama kwani linaweza kutokewa na matetemeko ya ardhi.

“Mkoa huu pamoja na maeneo yote yaliyo katika Ukanda wa Bahari hayako salama, kwani pia yanaweza kutokea na matetemeko ya ardhi,” alisema.

Kanda ya Ziwa, Kati

Mbali na Jiji la Dar es Salaam, Profesa Mruma alitaja Ukanda wa Ziwa Nyasa na hasa mikoa ya Ruvuma na Mbeya, ambako alisema kumepitiwa na Bonde la Ufa na kuna kitovu hicho, hivyo wakati wowote tetemeko linaweza kutokea.

Alisema katika Ziwa Rukwa, Mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani inaweza kupatwa na tetemeko hilo kupitia kitovu kilichoko katika ziwa hilo.

Mtaalamu huyo alisema Mkoa wa Kigoma nao uko hatarini kutokana na kitovu kilichoko katika Ziwa Tanganyika, huku Mkoa wa Kagera ukiwa hatarini kutokana na kitovu kilichoko katika Ziwa Albert, nchini Uganda.

Profesa Mruma aliutaja mkoa wa Dodoma kuwa nao upo hatarini kupata tetemeko la ardhi katika kitovu kilichoko kwenye Mlima Chinene.

Mkoa wa kumi

Profesa Mruma alisema hadi Julai 2007 Mkoa wa Arusha ulikuwa umepatwa na matetemeko 18 kutokana na kitovu kilichoko katika Milima ya Ol Doinyo Lengai, ambao wenyeji wake jamii ya Kimasai, wanautambua kuwa ‘Mlima wa Mungu’.

Pamoja na kutaja mikoa hiyo kumi, Profesa Mruma alihadharisha kuwa tetemeko la ardhi linalogusa Tanzania, linaweza pia kupata msukumo kutoka vitovu vilivyoko katika nchi jirani, hivyo si lazima kitovu kiwe Tanzania.

“Kuna eneo kama Ziwa Kivu katika nchi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ziwa Albert, Uganda na Kenya na Ethiopia, yakiwa na tetemeko yanagusa hadi kwetu,” alisema.

Dk Mshiu wa UDSM katika hilo, naye alisema hata maeneo ya jirani na kitovu cha tetemeko, yanaweza kuathirika.

Kwa mujibu wa Dk Mshiu, athari katika maeneo au mikoa ya jirani, husababishwa na uelekeo wa tetemeko kutoka katika kitovu, upande linakoelekea huathirika na eneo ambalo halikuelekea, hakutaathirika.

Ukubwa, upimaji

Akizungumzia ukubwa wa matetemeko ya ardhi yaliyokwishatokea nchini, Profesa Mruma alisema lililopiga Kagera si kubwa katika nchi, ingawa madhara yake ndiyo makubwa katika historia ya matetemeko nchini.

Tetemeko la Kagera kwa mujibu wa Profesa Mruma, lilikuwa na ukubwa wa uzito wa skeli ya Richter 5.7, wakati taarifa zinaonesha kuwa tetemeko kubwa lililowahi kutokea nchini, lilifikia uzito wa skeli ya Richter 6.3 na lilipiga mkoani Mtwara.

Alipoulizwa kwa nini tetemeko la Kagera limesababisha athari kubwa, wakati ni dogo ikilinganishwa na la Mtwara, Profesa Mruma alisema madhara yaliyotokea Kagera, yamechangiwa na nyumba nyingi kukosa ubora ikiwa ni pamoja na kutokuwa na linta.

Madhara mengine alisema yanaweza kuwa yametokana na ukosefu wa teknolojia ya kutoa taarifa za kutambua tetemeko wakati likitokea.

“Tetemeko linatokea kwa sekunde hali inayochangia taarifa zake kutojulikana pale linapotokea na hiyo ni moja ya sababu ya kuwep  madhara wakati mwingine.

“Teknolojia iliyopo duniani kwa sasa ni ile inayotoa taarifa muda huo huo tukio likitokea, pamoja na ukweli kuwa hakuna teknolojia inayoweza kutoa taarifa kabla ya tukio.

“Lakini sisi bado tupo katika mfumo wa zamani wa kukusanya taarifa na baadaye ndio tunazielezea kutokana na ukosefu wa mfumo wa mtandao kama walivyo wenzetu,” alisema Profesa Mruma.

Profesa Mruma alisema GST ina vituo tisa vyenye uwezo wa kukusanya taarifa baada ya tukio, hivyo mikakati yao ni kuhakikisha wanakuwa na teknolojia ya kisasa ya sateliti, iwasaidie kupata taarifa muda huo huo wakati tetemeko likitokea.

Kwa nini tetemeko linatokea?

Akijibu swali kuhusu kitu kinachotokea kitaalamu kabla ya tetemeko, alisema ni miamba ya chini ya ardhi kuteleza kutokana na mgandamizo na kuhama umbali wa Kilometa 10 hadi 40.

Profesa Mruma alisema tetemeko lililotokea Kagera lilitokea Kilometa 10 chini ya ardhi na kusababisha madhara yaliyotokea, lakini kama lingetokea Kilometa 40 madhara yangekuwa makubwa zaidi.

”Tetemeko hilo lililotokea Septemba 10 mwaka huu majira ya saa 9:27, mchana kitovu chake kilikuwa kati ya Latitudo 10 06’ na Longitudo 31055’ eneo ambalo ni Kilometa 20 Kaskazini Mashariki mwa Kijiji cha Nsunga na Kilometa 42 Kaskazini Magharibi mwa Mji wa Bukoba,” alisema Profesa Mruma.

Kujikinga

Akielezea namna ya kujikinga tetemeko linapotokea, Profesa Mruma alisema kwanza jamii inashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa kuzingatia viwango halisi vya ujenzi.  Amewataka wananchi kuweka misingi imara wakati wa ujenzi wa nyumba na kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo na kuepuka kujenga nyumba milimani.

Profesa Mruma alisema tetemeko likitokea, mahali salama ambako mwananchi anashauriwa kukaa ni sehemu ya wazi, isiyo na majengo marefu au miti mirefu au miinuko mikali ya ardhi.

“Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba, unashauriwa ukae chini ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta.

“Ukiwa ndani jiepushe kukaa karibu na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha, ili usiangukiwe na vitu hivyo,” alisema Profesa Mruma.

Wananchi pia wanashauriwa kuzima umeme katika majengo, ili kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme kama mitetemo itaendelea. Pia wametakiwa kukagua majengo kwa uangalifu na kuhakikisha hawapati madhara baada ya tetemeko na kama yanaweza kuendelea kutumika, ikibidi waite wataalamu wa majengo ili wayafanyie ukaguzi.

No comments:

Post a Comment

Sponsor