Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe
17 Septemba, 2016 amepokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na
tetemoko la ardhi lililotokea katika Mkoa wa Kagera na mikoa jirani ya
Geita, Mwanza na Mara kutoka kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Pamoja
na kupokea taarifa hiyo Rais Magufuli amepokea mchango wa fedha taslimu
kiasi cha Dola za Kimarekani laki mbili (USD-200,000/-) sawa na
takribani Shilingi za Kitanzania Milioni Mia nne na thelathini na saba
(Tshs-437,000,000/-) kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri
Kaguta Museveni na pia amepokea taarifa ya mchango wa mabati, blanketi
na magodoro vyenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 115 kutoka
kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia
waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.
Katika
taarifa yake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema tetemeko hilo
limesababisha vifo vya watu 17, majeruhi 440, nyumba 2063 zimeanguka,
nyumba 14,081 zipo katika hali hatarishi na nyumba 9,471 zimepata
uharibifu mdogo, huku watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
Mhe.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo
kupeleka chakula, huduma za matibabu na hifadhi za dharura kwa
waathirika na pia inaratibu ukusanyaji wa michango kutoka sehemu
mbalimbali ambapo mpaka sasa kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni
tatu nukta sita (Tshs Bilioni 3.6) zimepatikana.
Akizungumza
baada ya kupokea taarifa ya maafa na michango kwa ajili ya waathirika
wa maafa hayo, Rais Magufuli amewashukuru wote waliojitoa kusaidia
waathirika wakiwemo Marais Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Mhe.
Uhuru Kenyatta wa Kenya na Paul Kagame wa Rwanda ambao wamempigia simu
za kumpa pole na tayari wametoa misaada yao, na pia nchi mbalimbali,
mashirika, wafanyabiashara, watumishi wa umma na watu binafsi na amesema
michango hiyo ina umuhimu mkubwa katika kukabiliana na athari za maafa
haya.
Dkt.
Magufuli ametoa wito kwa Watanzania na wote walioguswa na maafa haya
kuendelea kutoa misaada kwa waathirika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, huku
akionya na kuvitaka vyombo vya dola kuwafuatilia watu wanaotaka kutumia
maafa haya kukusanya michango kwa lengo la kujinufaisha.
Rais
Magufuli amebainisha kuwa Serikali itahakikisha inarekebisha
miundombinu iliyoharibika zikiwemo shule, vituo vya matibabu, barabara
na huduma nyingine za kijamii na pia ametaka wananchi waliokumbwa na
madhara ya tetemeko hususani nyumba zilizobomoka, wajipange kurekebisha
nyumba zao kwa kuwa Serikali pekee yake haitaweza kujenga nyumba zote
zilizobomoka.
Aidha,
Rais Magufuli amewasihi Watanzania kuwapuuza watu wanaotaka kutumia
maafa haya kueneza uchonganishi na chuki dhidi ya Serikali na ameweka
wazi kuwa mpaka sasa hakuna teknolojia ya kutabiri kutokea kwa tetemeko
la ardhi na kwamba tetemeko hili halikuletwa na Serikali.
Dkt.
Magufuli amesema hata mataifa makubwa yenye maendeleo makubwa ya uchumi
na teknolojia yanakumbwa na tetemeko la ardhi na kusababisha vifo vya
idadi kubwa ya wananchi na uharibifu mkubwa wa mali.
“Nilikuwa
najaribu kuangalia kwa mfano nchi kama China kwenye mwaka 2014 watu 617
walipoteza maisha, Mwaka 2013 walipoteza watu 193, Mwaka 2010
walipoteza watu 2,998 Mwaka 2008 China ilipoteza watu 98,712.
Ukijaribu
kuangalia Japan, nchi ambayo imeendelea na ina utaalamu wa hali ya juu
sana, kwenye mwaka 2016 tarehe 14 mwezi wa nne ilipoteza watu 6, baada
ya siku mbili tarehe 16 mwezi wa nne 2016 tetemeko likatokea tena na
likaua watu 35, mwaka 2012 likaua watu 3, mwaka 2011 likaua watu 15,904
mwaka 2008 likaua watu 12, mwaka 2007 likaua watu 11, mwaka 2004 likaua
watu 40, mwaka 1923 liliua watu 142,800 na hiyo ni Japan. Amesisitiza
Rais Magufuli.
Shughuli
ya kupokea taarifa ya Waziri Mkuu na michango kwa ajili ya waathirika
wa tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera na Mikoa jirani
imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt Suzan
Kolimba, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Balozi wa Uganda
nchini Tanzania Mhe. Dorothy Hyuha na Naibu Balozi wa Kenya nchini
Tanzania Mhe. Boniface Muhia.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment